Magaidi 13 wengine waangamizwa Sinai Misri
Jeshi la Misri limetangaza habari ya kuangamizwa magaidi 13 katika muendelezo wa operesheni za wanajeshi wa nchi hiyo katika Rasi ya Sinai.
Jeshi la Misri limetangaza leo kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wameshambulia maficho 9 ya magaidi na kuyaangamiza. Mbali na kuua magaidi hao 13, jeshi hilo limefanikiwa pia kuwatia mbaroni magaidi wengine 86.
Limeongeza kuwa, wanajeshi wawili wa nchi hiyo wameuawa katika mapigano na magaidi hao na mwengine mmoja amejeruhiwa.
Tarehe 9 mwezi ulioisha wa Februari, jeshi la Misri lilianzisha operesheni kubwa ya kupambana na magaidi katika jangwa la Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Katika miaka ya hivi karibuni eneo la Sinai nchini Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya magaidi na operesheni za jeshi la nchi hiyo na hadi sasa makumi ya maafisa wa kijeshi na polisi wameshauawa. Mara kwa mara jeshi la Misri limekuwa kwa upande wake likitangaza habari za kuuawa magaidi wengi kwenye operesheni zake.
Katikati ya mwezi ulioisha wa Februari, jeshi la Misri lilitangaza habari ya kuua magaidi wasiopungua 12 na kuwatia mbaroni wengine 100 katika opereseheni kubwa inayoendelea kaskazini mwa Rasi ya Sinai.
Taarifa hiyo ya jeshi la Misri ilitolewa siku moja baada ya jeshi hilo kutangaza kwamba limeua magaidi 16 katika opesheni kama hiyo. Taarifa ya jeshi la Misri iliongeza kuwa, ndege za kivita za nchi hiyo zimeshambulia maeneo 60 yakiwemo magari, maghala ya silaha na vituo vya mawasiliano vya magaidi.