Wajumbe wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya wawasili Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4105-wajumbe_wa_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_ya_libya_wawasili_tripoli
Wajumbe wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa leo wamewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kupuuza maonyo yaliyotolewa na mirengo hasimu iliyowataka kutoukaribia mji huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 30, 2016 11:11 UTC
  • Wajumbe wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya wawasili Tripoli

Wajumbe wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa leo wamewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kupuuza maonyo yaliyotolewa na mirengo hasimu iliyowataka kutoukaribia mji huo.

Baraza la Urais la kuiongoza Libya liliundwa mwishoni mwa mwaka jana chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa katika jitihada za kuhatimisha machafuko ya kisiasa na mgogoro uliokuwa umeikumba nchi hiyo tangu baada ya vuguvugu lilimuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gadafi miaka mitano iliyopita.

Baraza hilo la Urais linatakiwa kuchukua nafasi ya serikali mbili hasimu ambazo zimekuwa zikipambana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, moia, yenye makao yake mjini Tripoli na nyengine iliyoko mjini Tobruk mashariki mwaka nchi hiyo.

Hivi karibuni, serikali iliyojitangaza mjini Tripoli ambayo haitambuliwi na Jamii ya Kimataifa, pamoja na makundi yanayobeba silaha yanayoiunga mkono zilitoa onyo la kutaka serikali ya Umoja wa Kitaifa isitie mguu wake katika mji mkuu huo wa Libya. Hata hivyo wajumbe saba wa Baraza la Urais akiwemo mkuu wake ambaye ni Waziri Mkuu mteule Fayez al-Sarraj, waliwasili mjini Tripoli leo kwa njia ya baharini na kuweka makao yao ya muda ya uongozi kwenye kituo cha jeshi la majini, baada ya kuzuiliwa kuingia mjini humo kwa kutumia njia ya anga na serikali hiyo hasimu.

Ali Abu Zakouk, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali iliyojitangaza mjini Tripoli amesema kuwepo kwa Sarraj "hakukubaliki". Vyombo vya habari vimeripoti kuwa hali ya mambo katika mji mkuu wa Libya ni "shwari" kufuatia habari za kuwasili wajumbe wa serikali ya Umoja wa Kitaifa.../