Mazungumzo ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Khalifa Haftar nchini Libya
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salamé amekutana na kufanya mazungumzo na Jenerali Khalifa Haftar kuhusiana na masuala ya kijeshi na kisiasa ndani ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili iliyopita ambapo Salamé anakutana na Haftar na kujadiliana naye kuhusu mchakato wa kisiasa nchini Libya. Kadhalika Salamé amekutana na Abdul-Rahman al-Abbar, meya wa mji wa Benghazi, na pande hizo mbili zimezungumzia hali ya kisiasa nchini humo na juhudi zilizofanyika kwa ajili ya kuimarisha usalama na amani nchini Libya.
Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Libya kumezidisha mapigano ya ndani na uwezekano wa kurejea tena baadhi ya makundi ya kigaidi nchini humo.
Vilevile kutokuwepo idara ya usalama na jeshi la taifa lenye nguvu, kumeyafanya baadhi ya maeneo ya Libya kuwa maficho na ngome za kuendeshea shughuli za uhalifu, magendo ya silaha, biashara ya dawa ya kulevya na hata magendo ya binadamu. Kwa upande mwingine ni kwamba, kuwepo silaha nyingi haramu na harakati za makundi ya waasi ni miongoni mwa sababu za kukosekana usalama na amani nchini Libya. Katika mazingira hayo, baadhi ya nchi za Kiarabu na nchi nyingine za Magharibi nazo zimezidisha ushawishi wao nchini humo kwa lengo la kutaka kuwa na nafasi kubwa zaidi katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.
Katika uwanja huo hivi karibuni Fayez al-Sarraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa ya Libya sambamba na kukosoa uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, alisema kuwa suala hilo limezidisha tofauti ndani ya Libya.
Ni kwa kutilia maanani hali hiyo ndiyo maana kunashuhudiwa mazungumzo na jitihada za kutafuta suluhisho la amani na mgogoro wa ndani wa Libya. Kufanyika uchaguzi na kuundwa serikali kuu yenye nguvu ni miongoni mwa njia muhimu zinazoweza kuiondoa Libya katika mkwamo na mizozo inayoshuhudiwa nchini humo. Katika uga huo Ghassan Salamé Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya mwezi Septemba mwaka jana aliwasilisha mpango wa kivitendo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuhitimisha machafuko na ghasia ndani ya nchi hiyo, mpango ambao uliunga mkono kufanyika kwa chaguzi za Bunge na Rais.
Hata hivyo hadi sasa bado hakujaandaliwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufanyika chaguzi hizo. Kuhusiana na suala hilo Salamé anasema: "Hivi sasa tayari tumefanikiwa kupiga hatua katika mchakato wa kuitisha zoezi la uchaguzi, nayo ni kuanza kuandikisha majina ya wapiga kura. hata hivyo raia wa Libya wanapaswa kwanza kupitishwa sheria ya uchaguzi na kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi huo”, mwisho wa kunukuu.
Licha ya juhudi zilizofanyika hadi sasa, lakini bado kunashuhudiwa mkwamo wa kisiasa nchini humo. Salahud-Din al-Jamali, mjumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu anasema: “Kwa sasa kunashuhudiwa hali ya mdororo nchini Libya. Hata hivyo watu wote wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya kufanikisha zoezi la uchaguzi”, mwisho wa kunukuu.
Katika mazingira hayo, vikao vya viongozi wa Libya na wale wa Umoja wa Mataifa bado vinaendelea. Inaonekana kwamba, hata mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Ghassan Salamé Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya na Khalifa Belqasim Haftar ni katika juhudi za kuandaa mazingira yatakayosaidia kuimarisha usalama na amani sambamba na kufanyika chaguzi za Bunge na Rais.