Kundi moja la kigaidi lasambaratishwa nchini Misri
(last modified Sun, 04 Mar 2018 17:06:42 GMT )
Mar 04, 2018 17:06 UTC
  • Kundi moja la kigaidi lasambaratishwa nchini Misri

Duru za usalama za nchini Misri zimetangaza habari ya kusambaratishwa kundi moja la kigaidi lenye mfungamano na Daesh (ISIS) katika mkoa wa Minya, kusini mwa mji mkuu Cairo.

Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi'i umezinukuu duru za kuaminika za Misri zikisema kuwa, vikosi vya kulinda usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kuangamiza kundi moja la magaidi wa Daesh karibu na Maghagha, kaskazini mwa mkoa wa Minya na kuwatia mbaroni wanachama wa kundi hilo.

Duru za usalama za Misri aidha zimesema, askari wa nchi hiyo wamegundua maficho ya kundi hilo la kigaidi na kukamata silaha na vifaa mbalimbali vya kijeshi pamoja na ramani za kushambulia vituo vya usalama na maeneo ya serikali, makanisa na watu muhimu jeshini.

Jeshi la Misri

 

Duru hizo aidha zimesema, kundi hilo lilikuwa na kambi maalumu ya mafunzo ya mashambulizi ya kigaidi karibu na mji wa Maghagha.

Hata hivyo matukio mengi ya kigaidi huwa yanatokea katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri ambako magenge mbalimbali yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maafisa usalama wa serikali, maeneo ya raia na hata misikiti.

Jeshi la Misri nalo limeanzisha kampeni kubwa ya kupambana na magaidi hao ambapo siku chache zilizopita lilitangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wameshambulia maficho 9 ya magaidi na kuyaangamiza. Mbali na kuua magaidi 13, jeshi hilo limefanikiwa pia kuwatia mbaroni magaidi wengine 86 katika operesheni hiyo.

Tags