Zaidi ya magaidi 100 wauawa katika Rasi ya Sinai nchini Misri
(last modified Fri, 09 Mar 2018 03:56:52 GMT )
Mar 09, 2018 03:56 UTC
  • Zaidi ya magaidi 100 wauawa katika Rasi ya Sinai nchini Misri

Msemaji wa jeshi la Misri ametangaza habari ya kuangamizwa zaidi ya magaidi mia moja katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kwenye jimbo la Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.

Tammer al Rahai alisema hayo jana na kuongeza kuwa, magaidi 105 wameshauawa tangu ilipoanza operesheni ya jeshi na polisi wa Misri dhidi ya magenge ya kigaidi katika Rasi ya Sinai.

Amesema, watu wengine 2,829 waliokuwa wakisakwa kwa tuhuma za uhalifu au kushirikiana na magaidi wametiwa mbaroni katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Hata hivyo amesema, baadhi yao wameshaachiliwa huru baada ya kuonekana hawana hatia.

Jeshi la Misri katika Rasi ya Sinai

 

Msemaji huyo wa jeshi la Misri aidha amesema, wanajeshi 16 wa nchi hiyo wameshauawa tangu ilipoanza operesheni hiyo ya kupambana na magaidi kaskazini mwa Misri na wanajeshi wengine 19 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa Tammer al Rahai, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, vikosi vya ulinzi vya Misri vimefanikiwa kugundua maficho 1,907 ya magenge ya kigaidi na maghala yao ya silaha na mada za miripuko.

Operesheni kubwa ya jeshi na polisi wa Misri dhidi ya magenge ya kigaidi ilianza tarehe 9 Februari 2018 katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hususan katika Rasi ya Sinai. 

Tags