Libya yashambulia meli ya kigeni katika mpaka wake wa baharini
Jeshi la Anga la Libya limesema kuwa, limeshambulia meli moja ya kigeni ambayo imeingia katika maji ya mashariki mwa nchi hiyo kinyume cha sheria.
Komandi ya operesheni ya Omar Mukhtar ya vikosi vya ulinzi vya Libya imetoa taarifa na kusema kuwa, meli hiyo ya kigeni ilishambuliwa jana Jumamosi baada ya kukaidi maonyo iliyopewa ya kurudi ilikotoka na kutoendelea kubakia kinyume cha sheria ndani ya mipaka ya majini ya Libya hivyo jeshi la anga la nchi hyo limelazimika kuishambulia.
Komandi hiyo ya Omar Mukhtar imesisitiza pia kuwa, meli hiyo imekamtwa na jeshi la anga na la majini la Libya na kupelekwa katika bandari ya Ra's al Hilal, mashariki mwa Libya.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, meli hiyo imekamatwa kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria katika umbali wa meli 14 ndani ya maji ya Libya na kufika hadi katika maeneo yaliyopigwa marufuku kuingia meli za kigeni.
Libya imekuwa na migogoro mingi na haijawahi kuwa na utulivu wala usalama tangu mwaka 2011 zilipoanza kampeni za kumpindua Kanali Muammar Gaddafi zilizokwenda sambamba na uingiliaji wa Marekani na muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO ambao baada ya kumpindua Gaddafi waliitelekeza nchi hiyo na kuacha silaha zikiwa zimetapakaa mikononi mwa watu na magenge ambayo kila moja hadi leo hii linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi nchini humo.
Mbali kuvamiwa na madola ya kigeni, Libya imekuwa ni njia kuu ya wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya kama ambavyo ni maficho ya magenge ya kigaidi ambayo baadhi ya wakati yanatuma katika nchi jirani na Libya kufanya uhalifu.