Rais wa Sudan aonana na Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Misri
Rais Omar al Bashir wa Sudan ameonana na Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Misri mjini Khartoum na kujadiliana naye masuala mbalimbali yanayozihusu nchi hizo mbili.
Mtandao wa habari wa al Yaum al Sab'i umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Abbas Mustafa Kaamil ameonana na Rais Omar al Bashir wa Sudan mjini Khartoum na pande mbili zimejadili changamoto muhimu za eneo lao na udharura wa kuwa macho na kutoruhusu changamoto hizo kuvuruga uhusiano wa nchi mbili jirani za Misri na Sudan.
Kabla ya kuonana na Rais al Bashir, ujumbe huyo wa Misri ulikuwa umeonana na Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Awadh Mohammd Ibn Auf, mjini Khartoum na pande mbili zilijadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kiusalama baina yao.
Uhusiano wa Misri na Sudan umeharibika zaidi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na masuala mbalimbali ukiwemo mzozo wa eneo la mpakani la Hala'ib, Shalateen na Aburamad.
Mzozo mwingine uliopo baina ya nchi hizo mbili ni ujenzi wa bwawa la al Nahdha la nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile na tuhuma za kila upande dhidi ya upande wa pili ambapo nchi mbili za Misri na Sudan zinatuhumiana kuwasaidia waasi wa upande wa pili. Mara kwa mara Sudan imekuwa ikiwashutumu viongozi wa Misri kuwa wanawaunga mkono waasi wa eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan.