Sudan: Tuko tayari kupanua ushirikiano wetu na nchi ya Qatar
Ibrahim Ghandour, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan amesema kuwa, nchi yake iko tayari kustawisha ushirikiano wake na nchi ya Qatar.
Ibrahim Ghandour amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Khartoum na Muhammad bin Abdul Rahman na kuishukuru serikali ya Doha kutokana na uungaji mkono wake kwa Khartoum na kubainisha kwamba, pande mbili zimefikia makubaliano ya kuunda kamati ya pamoja ya mashauriano ya kisiasa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan amesema kuwa, hati ya makubaliano ya Doha ilikuwa ndio njia pekee ya amani katika eneo la Darfur Sudan na kwamba, mazungumzo ya mawaziri wa mashauri ya kigeni wa pande mbili ni fursa ya kujadili tena suala hilo na kukamilisha juhudi zilizoanzioshwa huko nyuma hususan za kulikarabati upya jimbo la Darfur.
Sudan inatangaza utayari wake wa kuimarisha uhusiano wake na Qatar katika hali ambayo, nchi hiyo inakabiliwa na mashinikizo ya serikali ya Saudi Arabia inayoitaka ipunguze ushirikiano wake na serikali ya Doha.
Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudi Araba iliongoza nchi nyingine za Kiarabu za Misri, Imarati na Bahrain kuiwekea vikwazo vya angani, baharini na ardhini nchi ndogo ya Qatar na kukata kabisa uhusiano wao na Doha.
Mnamo tarehe 23 Juni, nchi hizo nne ziliipatia Qatar orodha ya masharti 13 na kutangaza kuwa kurejeshwa tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo kutategemea utekelezwaji wa masharti yote hayo na serikali ya Doha.
Masharti muhimu zaidi ambayo Saudi Arabia na washirika wake waliishurutisha Qatar ni kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran na Hizbullah ya Lebanon, kuifunga stesheni ya televisheni ya Aljazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki ndani ya ardhi ya Qatar. Serikali ya Doha imeyakataa masharti hayo.