Magaidi wa Daesh wanatumia kadi za simu za Israel nchini Misri
(last modified Wed, 14 Mar 2018 08:00:15 GMT )
Mar 14, 2018 08:00 UTC
  • Magaidi wa Daesh wanatumia kadi za simu za Israel nchini Misri

Mtandao mmoja wa Intaneti wa Israel umesema kuwa, magaidi wa genge la wakufurishaji la Daesh walioko katika jangwa la Sinai la kaskazini mwa Misri, wanatumia kadi za simu za mashirika ya Kizayuni kufanya operesheni zao ndani ya ardhi ya Misri.

Mtandao wa Globes wa Israel umesema hayo na kuongeza kuwa, magaidi wa ISIS wenye ngome zao kaskazini mwa Misri wanatumia kadi za simu za Israel na hivyo inakuwa ni vigumu kwa jeshi la Misri kufutailia nyendo zao na kupambana nao.

Mtandao huo umesema kuwa, jeshi la Misri limeamua kufunga mawasiliano ya kanali zote za simu za mkononi za Israel katika Rasi ya Sinai.

Aidha Misri ina wasiwasi kwamba magaidi wa Daesh wanatumia simu za mkononi kwa ajili ya kuripua mabomu yaliyotegwa masafa ya mbali.

Inadaiwa kuwa magaidi wa Daesh (ISIS) wanapenda sana kutumia simu aina ya Nokia kwa sababu mbalimbali

 

Hata hivyo mjumbe mmoja wa Baraza la Mawaziri la Israel amelalamikia uamuzi wa jeshi la Misri la kukata mawasiliano ya simu za mkononi za Israel katika Rasi ya Sinai na kudai kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuruka na ndege katika mipaka ya anga ya utawala wa Kizayuni. Viongozi wengine wa Israel nao wamelalamikia uamuzi huo na kusema kuwa, kukata mawasiliano ya simu za mkononi za Israel ni uhalifu.

Itakumbukwa kuwa katika operesheni yake ya kupambana na mgaidi wa Daesh, tarehe 21 Februari mwaka huu, jeshi la Misri lilishambulia kanali za simu za mkononi za Israel katika jangwa la Sinai. Mashambulizi hayo yaliathiri antena za kanali za simu za mkononi za Israel na kupelekea simu za watu laki tatu wanaotumia kadi za simu za Israel katika mpaka wa Misri na ardhi za Palesitna zinazokaliwa kwa mabavu kupata matatizo ya kukatika mawasiliano au kutopata huduma vizuri. 

Magaidi wa ISIS katika jangwa la Sinai nchini Misri

 

Tags