Mamia ya watu wameuawa au kutekwa nyara Libya mwaka jana 2017
Taasisi ya Haki za Binadamu ya "Mshikamano" ya nchini Libya imetoa ripoti ikieleza kuwa mwaka jana wa 2017 matukio 744 ya mauaji na utekaji nyara yaliripotiwa na kusajiliwa nchini humo.
Taasisi hiyo ya kutetea haki za binadamu imebainisha kuwa idadi hiyo ya watu walioripotiwa kuuawa au kutekwa nyara inajumuisha tu ripoti zilizowasilishwa na taasisi rasmi na zile za vyombo vya habari ambazo zimethibitishwa na vyanzo vyao vya habari na haziwajumuishi wahanga waliouawa katika mapigano ya kijeshi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 78 ya wahanga wa utekaji nyara au mauaji huko Libya ni raia wa kawaida.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa asilimia 89 ya jinai zimetekelezwa katika miji nane na asilimia 11 ya jinai zilizosalia zimetokea katika miji 37 na vitongojini. Mji wa Benghazi umekuwa na wahanga 144 wa utekaji nyara na mauaji nchini Libya, kiwango ambacho kinatajwa kuwa cha juu zaidi ikilinganisha na miji mingine ya nchi hiyo.
Habari nyingine kutoka Libya zinaeleza kuwa, watu 4500 wakazi wa mji wa Sabha kusini mwa nchi hiyo wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano ya karibuni katika mji huo.
Libya ilitumbukia katika mapigano na ukosefu wa amani tangu alipoondolewa madarakani dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.