Sudan yasema, ina azma ya kutatua hitilafu zake na Misri
(last modified Mon, 19 Mar 2018 15:22:36 GMT )
Mar 19, 2018 15:22 UTC
  • Sudan yasema, ina azma ya kutatua hitilafu zake na Misri

Rais wa Sudan amesema kuwa nchi yake imedhamiria kwa dhati kutatua hitilafu zilizopo kati ya Khartoum na Cairo.

Rais Omar al Bashir wa Sudan ambaye amefanya ziara huko Misri amesema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo huko Cairo kuwa wamekubaliana kuhusu suala la kuwezesha safari za raia na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi mbili hizo kupitia ujenzi wa barabara na njia za reli. 

Rais al Bashir amesema kuwa ipo irada kubwa ya kisiasa  kwa ajili ya kudumisha ushirikiano ili kuyapatia ufumbuzi masuala yote yanayozusha hitilafu kati ya nchi mbili hizo. 

Rais wa Sudan ameashiria pia uchaguzi wa Rais unaotazamiwa kufanyika hivi karibuni nchini Misri na kueleza uungaji wake mkono kwa Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo. 

Rais Abdel Fattah al Sisi pia ameeleza hatua zilizochukuliwa na Misri, Sudan na Ethiopia kwa ajili ya kutatua tatizo la bwawa la An Nahdhah na kusema kuwa: Wamefikia makubaliano ya kuitisha vikao vya mara kwa mara kwa lengo la kuboresha maslahi ya nchi mbili.

Bwawa la An Nahdhah nchini Ethiopia 

Uhusiano wa Misri na Sudan ulivurugika katika miezi kadhaa ya hivi karibuni kutokana na hitilafu zilizojitokeza kuhusu baadhi ya masuala ukiwemo mzozo wa Bwawa la An Nahdhah na tuhuma za Sudan dhidi ya Misri kwamba Cairo inawaunga mkono waasi katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.  

Tags