Mar 21, 2018 04:30 UTC
  • Amnesty: Nigeria haikujali tahadhari kuhusu utekaji nyara Dapchi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, askari usalama wa Nigeria hawakujali taarifa walizopewa zilizotahadharisha kwamba kundi la watu waliokuwa na silaha lilikuwa mbioni kuelekea katika mji ambako wasichana wasiopungua 110 wa shule walitekwa nyara mwezi uliopita wa Februari.

Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema jeshi na polisi ya Nigeria ilipewa tahadhari masaa kadhaa kabla ya shambulizi la Februari 19 lililopelekea kutekwa nyara zaidi ya wasichana 110 wa shule moja kaskazini mwa nchi hiyo.

Amnesty International imenukuu ushahidi uliotolewa na watu 23 ambao wameeleza jinsi watekaji nyara karibu 50 walivyowasili katika mji wa Dapchi, katika jimbo la Yobe wakiwa kwenye magari 8 na kuteka nyara wasichana hao. Watu hao wanasema jeshi la Nigeria halikuchukua hatua yoyote ila baada ya watekaji nyara kukamilisha shambulizi lao na kuondoka.

Mamia ya wasichana wa shule wametekwa nyara na kundi la Boko Haram, Nigeria

Tarehe 19 mwezi uliopita wa Februari wapiganaji wanaoaminika kuwa ni wa kundi la Boko Haram walishambulia shule moja ya wasichana katika eneo la Dapchi kwenye jimbo la Yobe na kuteka nyara wasichana 111. Hii ni mara ya pili kundi hili linashambulia shule ya wasichana nchini Nigeria. Aprili mwaka 2014 wapiganaji wa kundi hilo la Boko Haram walishambulia shule ya wasichana ya Chibok na kuteka nyara wasichana 276 na hadi sasa hatima ya zaidi ya mia moja kati yao haijulikani.      

Tags