Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaanza nchini Misri
Mashindano ya 25 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu yalianza jana Jumamosi tarehe 24 Machi, 2018 nchini Misri yakishirikisha wajumbe kutoka nchi 50 duniani.
Abdul Fattah Quswi, mjumbe wa jopo la maulamaa la Misri alisema katika ufunguzi wa mashindano hayo hiyo jana kwamba, shabaha ya kufanya mashindano hayo ni kurekebisha na kuonesha taswira sahihi kuhusu Qur'ani Tukufu na Uislamu baada ya magenge ya kigaidi kufanya jinai zilizoiharibia jina dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo zimehudhuriwa pia na Muhammad Mukhtar Jum'a, Waziri wa Wakfu wa Misri, wageni kutoka kona mbalimbali za dunia pamoja na jopo la majaji wa mashindano hayo.
Mashindano ya 25 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu nchini Misri yamefanyika kwa hima na usimamizi wa Wizara ya Wakfu ya nchi hiyo yakiwa na kaulimbiu ya kushikamana na Quds Tukufu yenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu hasa baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa Quds ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mashindano hayo yataendelea hadi siku ya Alkhamisi ya tarehe 29 Machi, 2018 na washindi watapewa zawadi nono.