EU yabainisha wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu nchini Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42192-eu_yabainisha_wasiwasi_wake_kuhusu_hali_ya_kibinadamu_nchini_kongo
Umoja wa Ulaya umeeleza wasiwasi wake kuhusu kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2018 23:53 UTC
  • EU yabainisha wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu nchini Kongo

Umoja wa Ulaya umeeleza wasiwasi wake kuhusu kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Christos Stylianides Kamishna Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Ulaya ambaye leo Jumatatu anatazamiwa kuhitimisha ziara yake ya siku tatu huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa Umoja wa Ulaya umekumbwa na wasiwasi mkubwa kutokana na  hali mbaya sana  ya kibinadamu huko Kongo. 

Christos Stylianides, Kamishna wa Umoja wa Ulaya Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu 

Umoja wa Ulaya unatazamiwa kuitisha Mkutano wa Wafadhili wa Kifedha kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo tarehe 13 mwezi ujao wa Aprili, hata hivyo nchi hiyo inaituhumu jamii ya kimataifa kwa kuzusha mikwaruzano na imepinga kushiriki katika mkutano huo. Kamishna huyo wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Ulaya ambaye leo Jumatatu anatazamia kuwa na mazungumzo huko Kinshasa na viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje ametangaza kuwa atajaribu kuwashawishi viongozi wa Kinshasa kuhusu udharura wa kushiriki mkutano huo wa Aprili 13 mjini Geneva Uswisi.  

Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ndizo zitakasosimamia mkutano huo kwa lengo la kukusanya msaada wa dola bilioni 1.7 kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.