Wamisri waanza uchaguzi wa Rais, al Sisi hakabiliwi na upinzani wa maana
Wamisri leo Jumatatu wameanza kupiga kura kumchagua Rais mpya katika uchaguzi wa rais usio na upinzani wa maana huku Abdel Fattah al Sisi akitazamiwa kuibuka mshindi baada ya serikali yake inayoungwa mkono na jeshi kuwafunga jela na kuwatisha wagombea wote wakuu waliokuwa wakitazamiwa kuchuana naye katika uchaguzi huu.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi kwa wakati wa Misri na zoezi la upigaji kura litaendelea kwa muda wa siku utatu chini ya hatua kali za usalama kote nchini humo.
Raia wa Misri milioni 60 waliotimiza masharti ya kupiga kura wanashiriki katika uchaguzi huu wa rais na matokeo rasmi ya uchaguzi yanatazamiwa kutangazwa Aprili Pili. Uchaguzi wa rais wa Misri unawashindanisha Abdel Fattah al Sisi na mpinzani wake pekee, Moussa Mostafa Moussa ambaye anatajwa kuwa muungaji mkono wa jenerali huyo mstaafu aliyegeuka na kuwa Rais wa nchi.
Katika miezi kadhaa ya kabla ya uchaguzi huu, shakhsia sita waliotazamiwa kushiriki uchaguzi wa leo wa Rais ama waliishia kutiwa mbaroni au waliamua kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho wakiashiria kuwepo vizuizi katika zoezi la kujiandikisha sambamba na kukandamizwa na vyombo vya usalama wa taifa.
Hasimu mkuu wa Rais Abdel Fattah al Sisi, jenerali wa zamani wa jeshi Sami Annan alitiwa mbaroni na jeshi siku kadhaa baada ya kutangaza azma ya kugombea kiti cha urais akituhumiwa kukiuka sheria za jeshi.