Al-Sisi ashinda uchaguzi tata Misri ulioshuhudia ushiriki mdogo
Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ameibuka mshindi wa uchaguzi tata wa rais uliofanyika Jumatatu iliyopita, kwa kuzoa asilimia 92 ya kura zote halali zilizopigwa.
Shirika rasmi la habari la serikali nchini humo MENA pamoja na magazeti ya serikali ya Al-Ahram na Akhbar el-Youm yametangaza kuwa, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa al-Sisi amepata ushindi wa kishindo, ingawaje uchaguzi huo umeshuhudia ushiriki mdogo wa wapiga kura.
Vyombo hivyo vya habari ya dola vimetangaza kuwa, watu milioni 23 kati ya milioni 60 waliotimiza masharti ya kupiga kura, sawa na asilimia 40 ya wapiga kura ndio walioshiriki katika zoezi hilo linaloonekana kususiwa kwa kiasi kikubwa na vyama vikuu vya upinzani.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Ahram, kura milioni mbili zimebatilishwa baada ya wapiga kura kuandika kwenye karatasi za kupigia kura, majina ya wagombeaji waliojiondoa au kuondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Nusra uchaguzi huo uwe na mgombeaji mmoja, yaani Abdul Fattah al-Sisi, lakini muungaji mkono wake Moussa Mostafa Moussa, alitangaza ghafla katika dakika za mwisho kuwa atachuana na al-Sisi katika uchaguzi huo.
Katika miezi kadhaa ya kabla ya uchaguzi huu, shakhsia sita waliotazamiwa kushiriki uchaguzi huo wa rais ama waliishia kutiwa mbaroni au waliamua kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho wakiashiria kuwepo vizuizi katika zoezi la kujiandikisha sambamba na kukandamizwa na vyombo vya usalama wa taifa.
Hasimu mkuu wa Rais Abdul Fattah al-Sisi, jenerali wa zamani wa jeshi Sami Annan alitiwa mbaroni na jeshi siku kadhaa baada ya kutangaza azma ya kugombea kiti cha urais akituhumiwa kukiuka sheria za jeshi.