Meya wa mji mkuu wa Libya, Tripoli atekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana
Kundi la watu wenye silaha limemteka nyara na kumpeleka kusikojulikana Meya wa mji mkuu wa Libya, Tripoli Abdulraouf Hassan Baitelmal.
Manispaa ya Tripoli imetoa taarifa leo na kueleza kuwa kundi la watu wenye silaha jana usiku lilivamia nyumba ya Baitelmal na kumteka nyara meya huyo wa mji mkuu huo wa Libya na kumpeleka kusikojulikana.
Sababu ya kutekwa nyara Abdulraouf Hassan Baitelmal hadi sasa bado haijajulikana.
Taarifa ya Manispaa ya mji wa Tripoli imesisitiza kuwa baraza hilo la mji wa Tripoli linasimamisha shughuli zake hadi itakapotolewa taarifa nyingine, kulalamikia kutekwa nyara meya huyo. Manispaa ya Tripoli imetoa wito kwa mamlaka husika na wakaazi wa mji mkuu huo wa Libya kufanya juhudi ili kuhakikisha Baitelmal anaachiliwa huru.
Manispaa ya Tripoli imeongeza kuwa vitendo vya aina hiyo vinatishia moja kwa moja kuwepo mfumo wa utawala na maisha ya kiraia.
Maafisa wa serikali wamekuwa wakieleza kwamba usalama hali ya usalama mjini Tripoli imeboreka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita; hata hivyo matukio ya utekaji nyara watu yameendelea kuwa kitu kilichozoeleka katika mji huo.
Tangu mwaka 2011 yalipotokea mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa kiongozi wa muda mrefu wa Libya Muammar Gaddafi, makundi ya wabeba silaha yamekuwa ndiyo yenye nguvu na mamlaka halisi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.../