Raia watano waliuawa Libya katika mapigano mwezi Machi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42530-raia_watano_waliuawa_libya_katika_mapigano_mwezi_machi
Idara ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, imetoa taarifa na kusema raia watano waliuawa na wengine 11 kujeruhiwa nchini Libya katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wa Machi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2018 02:57 UTC
  • Raia watano waliuawa Libya katika mapigano mwezi Machi

Idara ya Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, imetoa taarifa na kusema raia watano waliuawa na wengine 11 kujeruhiwa nchini Libya katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wa Machi.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili,  UNMSIL imesema raia hao waliuawa au kujeruhiwa katika vitendo vya ufyatuaji risasi, milipuko ya magari yaliyotegwa mabomu na kulipuka mabomu yaliyotegwa ardhini.

Idara hiyo ya Umoja wa Mataifa imetoa wito kwa pande hasimu nchini Libya kuacha kuvurumisha maroketi katika maeneo ya raia na pia kujizuia kuweka zana zao za kivita katika maeneo ya makazi ya raia. 

Libya ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwaka 2011 baada ya Marekani na majeshi ya NATO kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya utawala wa zamani wa nchi hiyo wakati ilipoanza harakati ya wananchi ya kutaka mageuzi.

Magaidi wa ISIS nchini Libya

Maeneo kadhaa ya nchi hiyo kwa sasa yanadhibitiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Hadi sasa serikali ya umoja wa kitaifa haijaundwa nchini humo kutokana na mivutano iliyopo kati ya makundi tofauti ya kisiasa huku kukiwa na serikali mbili hasimu moja ikiwa katika mji mkuu, Tripoli, na nyingine katika mji wa mashariki wa Tobruk. Jitihada za kieneo na kimatiafa za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Libya zimefeli hadi sasa.