Viongozi wa Chadema Tanzania waachiwa huru kwa dhamana
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nchini Tanzania imewaachia huru kwa dhamana viongozi 6 wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Masharti ya dhamana yao ilikuwa ni kusaini bondi ya Shilingi milioni 20 za Tanzania sawa na takriban dola 10,000 za Marekani, na kuwa na wadhamini wawili wenye barua kutoka ofisi za serikali za mitaa au vijiji.
Kadhalika viongozi hao wa upinzani Tanzania wametakiwa kuripoti kituo kikuu cha polisi kila siku ya Alkhamisi.
Mbali ya Mbowe wengine ni Katibu Mkuu Dkt Vicent Mashinji, manaibu katibu wakuu John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa. Wengine ni Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake wa chama hicho, Ester Matiko na Mwenyekiti wake, Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, wote wakikabiliwa na kesi ya jinai, wakidaiwa pamoja na mambo mengine kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali.
Machi 29, viongozi hao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walinyimwa dhamana na Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri kwa kuwa hawakuwa wametimiza masharti. Watuhumiwa hao walikuwa mahabusu tangu walipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo Machi 27 mwaka huu.
Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 16, mwaka huu 2018.