Kiongozi wa upinzani Sierra Leone ajitangaza mshindi wa urais
Jeshi la Sierra Leone limekadhibisha tuhuma za kula njama ya kumuua kiongozi wa upinzani nchini humo, Brigedia Julius Maada Bio ambaye anadai kuwa ameibuka mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais.
Taarifa iliyosainiwa na Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, B. Sesay imesema kuwa, jeshi hilo limesikitishwa mno na madai mazito ya urongo yaliyotolewa na Umaru Napolean Koroma, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Sierra Leone People's Party SLPP, kwamba linapanga njama ya kumuua kiongozi wa upinzani, Maada Bio.
Chama cha upinzani cha SLPP kimedai kuwa, kwa mujibu wa ujumlishaji wa kura uliofanywa na maajenti wake, kiongozi wake Maada Bio ameibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 54.4 ya kura, na kwamba mgombea wa kiti hicho kupitia muungano tawala wa APC, Samura Kamara amepata asilimia 45.8 ya kura zote halali zilizopigwa.
Hii katika hali ambayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC inatazamiwa kutoa matokea rasmi ya duru ya pili ya urais Alkhamisi ijayo.
Kwa mujibu wa tume hiyo ya uchaguzi, katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, Samura Kamara alipata kura milioni moja na elfu 83 sawa na asilimia 42.7 huku mpinzani wake Julius Maada Bio akipata kura milioni moja na elfu 97, sawa na asilimia 43 ya kura zote.
Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini humo ilifanyika tarehe saba ya mwezi uliopiota ambapo wagombea 16 walichuana.