Morocco yaitaka UN na Algeria kubeba dhima ya harakati za Polisario
Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco ameutaka Umoja wa Mataifa na taifa la Algeria kubeba dhima ya mashambulizi ya Harakati ya Kupigania Ukombozi wa Sahara Magharibi Polisario.
Nasser Bourita ameyasema hayo alipokutana na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani ambapo sambamba na kumkabidhi barua kutoka kwa Mfalme Mohammed VI wa Morocco alitahadharisha kwamba endapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitotekeleza majukumu yake kuhusiana na suala hilo, basi Rabat italazimika kuchukua hatua katika uwanja huo.
Nasser Bourita amesisitiza kuwa, vitendo vinavyokinzana na sheria vya harakati hiyo ya Polisario, ni hatari kwa mkataba wa usitishaji vita na vinakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kama ambavyo pia vinadhoofisha mwenendo wa kisiasa katika eneo hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco ameongeza kuwa, Algeria imekuwa ikiliunga mkono wa kifedha na kidiplomasia eneo la Polisario sambamba na kuwapa hifadhi viongozi wake, katika hali ambayo Rabat imekuwa ikiitaka Algiers kuishirikisha katika suala hilo.
Inafaa kuashiria kuwa, mwaka 1975 eneo la Sahara Magharibi lililokuwa chini ya mkoloni Muhispania liliunganishwa na Morocco huku harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria ikitaka kujitenga eneo tajwa. Kwa sasa Polisario inadhibiti asilimia 20 hadi 25 tu ya ardhi yote ya Sahara Magharibi.