Libya kuitisha kongamano la kitaifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42730-libya_kuitisha_kongamano_la_kitaifa
Viongozi wa Libya wako mbioni kuandaa utangulizi wa mkutano wa kitaifa wenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 06, 2018 14:11 UTC
  • Libya kuitisha kongamano la kitaifa

Viongozi wa Libya wako mbioni kuandaa utangulizi wa mkutano wa kitaifa wenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa zaidi kutoka nchini Libya zinasema kuwa, kunafanyika juhudi  za kuhakikisha kuwa, mkutano huo wa kitaifa unafanyika katika miji ya Zuwarah na Bengazi.

Kamati yenye jukumu la kuandaa kongamano hilo la kitaifa imetangaza kuwa, kikao cha mashauriano chenye lengo la kuandaa utangaulizi wa mkutano huo wa kitaifa kimekwishafanyika na kwamba, mikutano kama hiyo inatarajiwa kuendelea hadi Juni mwaka huu.

Imeelezwa kuwa, lengo la vikao na mikutano hiyo ya mashauriano ni kuhakikisha kwamba, kongamano lijalo la kitaifa la Libya linazishirikisha pande zote na hivyo maamuzi yake kuwa na taathira.

Machafuko nchini Libya yameiharibu vibaya nchi hiyo

Kongamano lijalo la kitaifa la Libya ni sehemu ya mpango wa Ghassan Salamé mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alioupendekeza mwishoni mwa mwaka jana ikiwa ni katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.

Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 baada ya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kuingia kijeshi katika nchi hiyo ikiwa ni katika kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imeendelea kushuhudia vurugu na ukosefu wa amani na hivyo kuifanya hali ya nchi hiyo kuwa mbaya siku baada ya siku.