Tunisia yawazuia wanamichezo wa Israel kuingia nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42790-tunisia_yawazuia_wanamichezo_wa_israel_kuingia_nchini_humo
Mahakama moja nchini Tunisia imewapiga marufuku wanamichezo wa taekwondo wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuingia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2018 22:48 UTC
  • Tunisia yawazuia wanamichezo wa Israel kuingia nchini humo

Mahakama moja nchini Tunisia imewapiga marufuku wanamichezo wa taekwondo wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuingia nchini humo.

Vuguvugu la kupinga kufanywa wa kawaida uhusiano wa Tunisia na Israel liitwalo National Commission for Supporting Arab Resistance and Opposing Normalisation and Zionism lilienda mahakamani kumshtaki Rais wa Shirikisho la Taekwondo nchini humo, Ahmed Gaaloul, likitaka asiruhusiwe kuwaalika wanamichezo hao wa Israel kushiriki mashindano ya mchezo huo katika eneo la Hammamet mwezi huu wa Aprili.

Sofiane Selliti, Msemaji wa Mwendesha Mashitaka katika kesi hiyo ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kuwa, Shirikisho la Taekwondo limepigwa marufuku kuwaalika, kuwapokea au kuwa mwenyeji wa wanatakekwondo wanne wa Kizayuni ambao walitazamiwa kushiriki mashindano hayo yanayomalizika Aprili 13.

Wananchi wa Tunisia katika maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina

Mwezi Februari mwaka huu, mamia ya wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchini Tunisia walifanya maandamano wakilitaka bunge la nchi hiyo lifanye haraka kupitisha sheria ambayo itatamka wazi kuwa ni uhalifu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kuilaani vikali Israel na kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.