Jeshi la Misri laua magaidi wanne Rasi ya Sinai
Jeshi la Misri linasema limewaua magaidi wane na kuwakamata wengine wengi katika oparesheni maalumu za kuwatimua magaidi walio katika eneo la Rasi ya Sinai.
Katika taarifa Jumapili, Jeshi la Misri limesema magaidi wawili na washukiwa wengine 250 wa uhalifu ambao walikuwa wakisakwa wametiwa mbaroni katika siku za hivi karibuni eneo hilo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zaidi ya magaidi 100 na wanajeshi 22 wa Misri wameuawa katika oparesheni zilizoanza Rasi ya Sinai miezi miwili iliyopita kufuatia amri ya Rais Abdel Fattah el-Sisi ambaye alitoa muhula wa miezi mitatu wa kuangamizwa makundi yanayofungamana na magaidi wakufurishaji wa ISIS eneo hilo.
Kwa miaka mingi sasa jeshi la Misri limekuwa likipambana na magenge yenye silaha katika Rasi ya Sinai. Mwezi Novemba 2017, watu wasiopungua 235 waliuawa katika shambulizi la bomu na risasi lililofanywa na magaidi dhidi ya Waislamu waliokuwa wanasali katika msikiti wa mji wa Bir al Abed wa jimbo la Sinai Kaskazini huko Misri.
Jeshi la Misri limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na vikosi vya ulinzi kwa ajili ya kuwaangamiza magaidi ambao wamekuwa wakihatarisha usalama katika Rasi ya Sinai. Makundi ya kigaidi yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika Peninsula ya Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.