Human Rights Watch yaitaka Misri iheshimu haki za binadamu
(last modified Wed, 11 Apr 2018 13:42:04 GMT )
Apr 11, 2018 13:42 UTC
  • Human Rights Watch yaitaka Misri iheshimu haki za binadamu

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limemtaka Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri kuhakikisha kuwa uvunjaji wa haki za binadamu unakomeshwa nchini mwake katika kipindi cha pili cha urais wake.

Gazeti la al Ra'i al Yaum limemnukuu Sarah Leah Whitson, mkurugenzi wa kitengo cha Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini cha shirika la Human Rights Watch akikosoa vikali mchakato wa kampeni za uchaguzi huko Misri na kumtaka Rais Abdul Fattah el Sisi abadilishe mwenendo wake.

Rais wa Misri, Jenerali Abdul Fattah el Sisi

 

Shirika hilo la haki za binadamu pia limegusia namna wanaharakati wa kisiasa wanavyosakamwa na vyombo vya mahakama na kupigwa marufuku kutoka nchini humo au kuporwa na kuzuiwa mali zao pamoja na za wanaharakati wa haki za binadamu na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuacha kuwapa mateso bali iwaachilie huru wafungwa wote wa kisiasa na waandishi wa habari waliotiwa mbaroni sambamba na kufungua uwanja mpana zaidi wa uhuru wa kujieleza.

Rais Abdul Fattah el Sisi alitangazwa tena mshindi wa asilimia 97 ya kura katika kipindi cha pili cha kugombea urais huko Misri uchaguzi ambao jamii ya kimataifa inasema umekosa vigezo vya demokrasia na ulikuwa wa kimaonyesho tu.

Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kilichofanyika nchini Misri si uchaguzi bali ni mchezo tu wa kisiasa uliofanyika kwa ajili ya kuendeleza udikteta na kuteswa wafungwa na wapinzani wa serikali huko Misri.

Tags