Rais wa Niger ameapishwa leo
Rais wa Niger ameanza rasmi kazi zake katika kipindi kingine cha urais baada ya kula kiapo leo Jumamosi.
Mahamadou Issoufou amekula kiapo leo katika sherehe maalumu baada ya kutangazwa mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi uliosusiwa na vyama vya upinzani.
Marais wa nchi 10 za Afrika wameshiriki kwenye sherehe hizo. Vyama vya upinzani vimesusia kushiriki kwenye sherehe hizo.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Niger, Mahamadou Issoufou amepata ushindi wa asilimia 95 ya kura za uchaguzi wa tarehe 20 mwezi uliopita wa Machi.
Vyama vya upinzani vinailaumu serikali kwa kufanya udanganyifu mkubwa kwenye uchaguzi kwa faida ya Mahamadou Issoufou.
Rais wa Niger amesema baada ya kula kiapo leo kuwa, ataunda serikali ya umoja wa kitaifa na yuko tayari kushirikiana na wapinzani kwa faida ya nchi na wananchi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.