Majina ya mawaziri wapya Libya kuwasilishwa bungeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43-majina_ya_mawaziri_wapya_libya_kuwasilishwa_bungeni
Majina ya mawaziri wapya wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya yatawasilishwa mbele ya bunge linalotambuliwa kimataifa ndani ya muda wa siku 10.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2016 21:45 UTC
  • Majina ya mawaziri wapya Libya kuwasilishwa bungeni

Majina ya mawaziri wapya wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya yatawasilishwa mbele ya bunge linalotambuliwa kimataifa ndani ya muda wa siku 10.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu mteule, Fayez al-Sarraj siku moja baada ya bunge la Tobrouk kuyakataa majina ya mawaziri waliokuwa wamependekezwa na Umoja wa Mataifa. Wabunge 89 kati ya 104 walipiga kura ya kuikataa serikali iliyokuwa imependekezwa na UN wakisema idadi ya mawaziri ilikuwa kubwa mno.

Bunge la pili la Libya ambalo halitambuliwi kimataifa na ambalo lina makao yake katika mji mkuu Tripoli pia limekataa kutambua serikali ya umoja wa kitaifa iliyokuwa imependekezwa na mjumbe maalumu wa umoja wa mataifa katika masuala ya Libya, Martin Kobler.

Wachambuzi wanasema Umoja wa Mataifa uliharakisha mchakato wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya kutokana na mashinikizo ya nchi za Ulaya na Marekani baada ya shambulizi la kigaidi mjini Paris, Ufaransa miezi miwili iliyopita.

Libya ambayo imegeuka uwanja wa mapigano na pango la magaidi imeshuhudia mapigano na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu kuangushwa utawala wa dikteta wa zamani, Muammar Gaddafi mwaka 2011.