Rais wa Misri arefusha hali ya hatari kwa miezi mingine mitatu
(last modified Sat, 14 Apr 2018 07:01:50 GMT )
Apr 14, 2018 07:01 UTC
  • Rais wa Misri arefusha hali ya hatari kwa miezi mingine mitatu

Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ametangaza kurefusha muda wa hali ya hatari nchini humo kwa miezi mitatu mingine ambao ulianza kutekelezwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya kujiri mashambulizi makubwa dhidi ya makanisa.

Rais al-Sisi ametoa tangazo hilo katika dikrii iliyochapishwa leo Jumamosi katika gazeti rasmi la serikali. 

Hali ya hatari ilianza kutekelezwa mwezi Aprili mwaka jana nchini Misri kufuatia kujiri mashambulizi mawili makubwa katika makanisa ya Wakristo wa Kikopti katika miji miwili ya Tanta na Alexandria kaskazini mwa Misri ambapo watu 45 walipoteza maisha. 

Haya yanajiri wiki mbili baada ya al-Sisi kutangazwa mshindi wa uchaguzi tata wa rais uliofanyika kati ya Machi 26 na 28, kwa kuzoa asilimia 92 ya kura zote zilizopigwa.

Askari usalama wa Misri

Hata hivyo uchaguzi huo ulikosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kutoshirikisha wagombeaji wa upinzani, ambao ima walitishiwa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro au walikamatwa na kuzuiliwa kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Hata hivyo al-Sisi alichuana na mpambe wake Moussa Mostafa Moussa wa chama cha al Ghad ambaye alichomekwa kwenye kinyang'anyiro hicho ili kuhalalisha zoezi la uchaguzi huo.
 

Tags