Magaidi waitishia serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4387-magaidi_waitishia_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_ya_libya
Kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa Sirte huko kaskazini mwa Libya ametishia kuishambulia serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2016 02:51 UTC
  • Magaidi waitishia serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya

Kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa Sirte huko kaskazini mwa Libya ametishia kuishambulia serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.

Abu Abdullah al Masri ametishia kuishambulia serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na kuituhumu kuwa ni serikali ya jeshi la Msalaba.

Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imeundwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya makundi ya Walibya katika mji wa Sakhirat nchini Morocco mwezi Disemba mwaka jana chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa anafanya juhudi ili kupata kura za kuwa na imani naye za wabunge wa nchi hiyo, hata hivyo bunge hilo limekataa kumpigia kura za kumuunga mkono.

Hii ni katika hali ambayo wananchi wa Libya walikuwa na matarajio haya kwamba kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ungekuwa mwanzo wa kupatikana uthabiti wa kisiasa na kurejeshwa amani nchini humo. Wakati huo huo magaidi wa kundi la Daesh wamefanikiwa kusonga mbele na kuteka baadhi ya maeneo ya Libya kwa kutumia vibaya pengo la madaraka lililopo nchini humo. Umoja wa Mataifa na taasisi ya kutetea haki za binadamu zimetahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu huko Libya kutokana na kuendelea hitilafu kati ya makundi hasimu.