Tishio la magaidi dhidi ya serikali ya Umoja wa kitaifa nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4399-tishio_la_magaidi_dhidi_ya_serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_nchini_libya
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh la mjini Sirte, kaskazini mwa Libya, limetishia kuishambulia serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Abu Abdullah al-Misri, kiongozi wa genge hilo la kigaidi mwenye makao yake mjini Sirte, ametishia kufanya shambulio dhidi ya serikali hiyo mpya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2016 07:16 UTC
  • Tishio la magaidi dhidi ya serikali ya Umoja wa kitaifa nchini Libya

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh la mjini Sirte, kaskazini mwa Libya, limetishia kuishambulia serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Abu Abdullah al-Misri, kiongozi wa genge hilo la kigaidi mwenye makao yake mjini Sirte, ametishia kufanya shambulio dhidi ya serikali hiyo mpya.

Aidha ameitaja serikali hiyo ya umoja wa kitaifa kuwa ni 'serikali ya kimsalaba'. Serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya iliundwa mwezi Disemba mwaka jana huko mjini Skhirat, nchini Morocco chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Hivi sasa Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu na Rais wa Baraza la Uongozi wa serikali hiyo, ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa, anafanya juhudi kubwa kuvutia uungaji mkono wa wajumbe wa bunge la taifa nchi hiyo, ingawa bado bunge hilo linaonekana kusita kutoa uungaji huo mkono kwa serikali hiyo mpya. Hii ni katika hali ambayo raia wa Libya walitarajia kwamba kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, ungekuwa mwanzo wa kurejeshwa uthabiti wa kisiasa na amani nchini. Wakati huo huo, magaidi wa kundi la Daesh sanjari na kutumia vibaya mwanya uliojitokeza wa kukosekana serikali yenye nguvu na kadhalika kuendelea mapigano kati ya makundi tofauti ya upinzani, limezidi kusonga mbele na kutunisha misuli yake katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Mvutano huo unendelea katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa na asasi zinazojihusisha na masuala ya haki za binaadamu, kwa pamoja zimeonya juu ya hali mbaya ya kibinaadamu nchini Libya. Kufuatia hali hiyo, baadhi ya nchi zinazojinadi kuwa eti ni vinara wa haki za binaadamu kama vile Uingereza, zimeonyesha kukerwa na pendekezo la jamii ya kimataifa la kupewa Libya kiasi cha fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake muhimu. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, msaada wa kifedha wa serikali ya Uingereza kwa ajili ya ukarabati wa Libya baada ya vita na machafuko ya tangu mwaka 2011 ni mdogo mara 13 zaidi ikilinganishwa na kiasi ilichokitumia wakati wa kujiri mashambulizi ya anga nchini Libya. Mwezi Machi mwaka huu, Martin Kobler, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alisema hali ya mambo nchini humo ni mbaya sana na hasa kwa kuzingatia bajeti ndogo ya jamii ya kimataifa kwa ajili ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Mbali na hayo idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo wamekimbilia nchi jirani tangu yalipoibuka mapinduzi ya wananchi hapo mwaka 2011. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu Walibya 5000 wapo nchini Algeria hadi sasa. Hivi karibuni pia nchi za Ufaransa, Italia, Uingereza na Marekani zilionyesha wasi wasi wao kutokana na hali mbaya nchini Libya.