UN yazitaka Morocco na Polisario kuvumiliana
Mgogoro baina ya serikali ya Morocco na harakati ya Polisario inayopigania uhuru wa eneo la Sahara Magharibi umemlazimisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuzitaka pande hizo mbili kustahamiliana na zijiepushe na jambo lolote linaloweza kuzusha machafuko katika eneo hilo.
Mwito huo wa António Guterres umekuja baada ya harakati ya Polisario kuamua kufanya mazoezi makubwa ya kijeshi katika eneo la Tifariti, suala ambalo linaweza kuzidisha mgogoro baina ya serikali ya Morocco na harakati hiyo.
Guterres amesema katika tamko lake hilo lililotangazwa na msemaji rasmi wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, kwamba, umoja huo unayafuatilia kwa karibu na kwa kina matukio ya Sahara Magharibi.
Umoja wa Mataifa pia umezitaka pande hizo mbili kutoharibu juhudi zinazoendelea za kufufua mazungumzo ya amani.
Mwito huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umetolewa katika hali ambayo Jumatatu iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco ilitoa tamko ikiutaka ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Sahara Magharibi kutekeleza vizuri jukumu lake kuhusu kile kilichosemwa na wizara hiyo kuwa ni uvunjaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusimamisha vita unaofanywa na harakati ya Polisario.
Mapigano baina ya harakati ya Polisario na serikali ya Morocco yalianza mwaka 1975 na yalisimama mwaka 1991 kutokana na mapatano maalumu yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa.