Upinzani Burundi waenda mahakamani kupinga matokeo ya kura ya maoni
Muungano wa upinzani nchini Burundi unaoongozwa na Agathon Rwasa jana Alkhamisi ulienda mahakamani kupinga matokeo ya kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, yaliyoipa ushindi kambi ya serikali.
Hii ni baada ya serikali ya Bujumbura kuwataka wanasiasa wa upinzani nchini humo kutumia njia za kisheria kuwasilisha malalamiko yao kupinga matokeo hayo badala ya kulalamika mbele ya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, kambi ya serikali ilishinda kura hiyo kwa kuzoa asilimia 73 ya kura, kwa maana kwamba Warundi 'waliunga mkono kwa kura ya ndio' kufanyika kwa marekebisho ya katiba ambayo yanampa baraka Rais Pierre Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034.
Pierre Célestin Ndikumana, wakili wa muungano wa upinzani wa Amizero y'Abarundi amesema, "Tumelazimika kwenda katika Mahakama ya Katiba kupinga namna zoezi hilo (la kura maoni) lilivyoendeshwa na mazingira ya kabla na wakati wa zoezi hilo, kulifanyika uchakachuaji mkubwa wa matokeo."
Kura hiyo ya maoni ya marekebisho ya Katiba ambayo kampeni zake zililalamikiwa na wapinzani wanaosema zilijaa vitisho dhidi yao, ilifanyika siku chache tu baada ya kutokea mauaji makubwa katika mji wa Cibitoke na kuzua wasiwasi mkubwa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema kwa akali watu 15 waliuawa wakati wa kampeni hizo, mbali na kesi sita za ubakaji na nane za utekaji nyara kunakiliwa.