Serikali ya umoja wa kitaifa Libya yachagua kiongozi
Baraza Kuu la Uongozi la serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya limemchagua Abdulrahman Al-Shater kuwa mkuu wa baraza hilo.
Abdulrahman Al-Shater, ambaye ndiye mjumbe mwenye umri mkubwa zaidi katika Baraza la Uongozi la serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, amechaguliwa kuwa mkuu wa baraza hilo katika uamuzi uliopitishwa na wajumbe hapo jana.
Mara baada ya kuchaguliwa, Al-Shater alisema, kupambana na ugaidi na machafuko ya kikaumu, kimadhehebu na kikabila ni miongoni mwa vipaumbele vikuu na malengo yatakayofanyiwa kazi na baraza hilo.
Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi la serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya aidha amevitaka vyama vya siasa na pande zinazopigana kufikiria juu ya kujenga nchi yenye ustawi na iliyoungana.
Libya ingali inashuhudia mapigano na machafuko baada ya kupita miaka mitano tangu alipoondolewa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gadafi.../