Mahakama yatupilia mbali kesi ya upinzani kuhusu kura ya maoni Burundi
Mahakama ya Katiba ya Burundi imetupilia mbali kesi iliyowasilisha na muungano wa upinzani nchini humo kupinga matokeo ya kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, yaliyoipa ushindi kambi ya serikali.
Uamuzi huo uliotolewa leo Alkhamisi na mahakama hiyo ambayo ndiyo ya juu kabisa nchini humo unamaanisha kuwa, kambi ya serikali ilishinda kihalali kura hiyo kwa kuzoa asilimia 73 ya kura, kama ilivyotangaza Tume ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi Burundi, asilimia 73 ya wapiga kura milioni 4.3 katika zoezi hilo waliunga mkono kwa kura ya ndio kufanyika kwa marekebisho ya katiba, ambayo yanampa baraka Rais Pierre Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034.
Pierre Célestin Ndikumana, wakili wa muungano wa upinzani wa Amizero y'Abarundi alisema walilazimika kwenda katika Mahakama ya Katiba kupinga namna zoezi hilo la kura maoni lilivyoendeshwa na mazingira ya kabla na wakati wa zoezi hilo, huku akisisitiza kuwa kulifanyika uchakachuaji mkubwa wa matokeo.
Nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika imekuwa katika mgogoro wa kisiasa tokea Aprili mwaka 2015, baada ya Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais ambapo wapinzani walisema ni kinyume cha sheria. Muhula huu unamalizika mwaka 2020, lakini marekebisho ya katiba yanampa kibali cha kugombea mihula mingine miwili ya miaka saba saba.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 1,200 wameuawa tokeo wakati huo hadi sasa.