Wahajiri haramu 221 waondolewa nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45246-wahajiri_haramu_221_waondolewa_nchini_libya
Idara ya wahajiri na wahamiaji nchini Libya imetangaza habari ya kuondolewa wahajiri haramu 221 nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 01, 2018 00:55 UTC
  • Wahajiri haramu 221 waondolewa nchini Libya

Idara ya wahajiri na wahamiaji nchini Libya imetangaza habari ya kuondolewa wahajiri haramu 221 nchini humo.

Idara ya Uhamiaji ya Libya imesema katika taarifa yake kwamba idara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji imefanikiwa kuwarejesha nyumbani kwa ndege raia 163 wa Somalia waliokuwa wanaishi nchini Libya kinyume cha sheria.

Taarifa ya idara hiyo imeongeza kuwa wahamiaji wengine 30 raia wa Bangladesh na 28 raia wa Pakistan nao wamesharejeshwa katika nchi zao.

Mapigano baina ya makukndi hasimu ni jambo la kawaida nchini Libya

 

Libya ni kituo kikuu cha wahamiaji haramu hasa wa Kiafrika wanaokimbilia barani Ulaya. Hata hivyo kuna idadi kubwa pia ya wahajiri kutoka nchi nyingine kama za Mashariki ya Kati na magharibi mwa Asia ambao nao wanaitumia Libya katika kituo kikuu cha kwenda kutafuta maisha barani Ulaya.

Magenge ya kigaidi na ya magendo ya binadamu yanatumia ukosefu wa amani na kutokuweko serikali kuu yenye nguvu nchini Libya kufanya uhalifu wao.

Kila mwaka makumi ya wahamiaji haramu wanasafirishwa hadi nchini Libya na magenge hayo yanayochukua fedha nyingi kutoka kwa wahajiri hao haramu ambao wengi wao huzama baharini au huangukia mikononi mwa makundi ya kigaidi na ya wahalifu na wengine hupigwa mnada na kuuzwa kama watumwa katika masoko ya Libya.