Jeshi la Taifa la Libya ladhibiti asilimia 75 ya mji wa Derna
Vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar vimetangaza kuwa vimeshafanikiwa kukomboa asilimia 75 ya mji wa Derna wa mashariki mwa nchi hiyo.
Televisheni ya Rusia al Yaum imemnukuu Ahmad al Massmari, msemaji wa Jeshi la Taifa la libya (LNA) akiwaambia waandishi wa habari mjini Benghazi kwamba vikosi vya jeshi hilo vimefanikiwa kukomboa zaidi ya robo tatu ya mji wa Derna. Vile vile amewataka wakazi wa mji huo kukaa mbali na maeneo ya mapigano ili kulirahisishia kazi Jeshi la Taifa la Libya.
Amesema, mali za wakazi wa mji wa Dena zitalindwa na vikosi vya Khalifa Haftar hivyo wakazi hao hawana haja ya kuwa na wasiwasi na mali zao, bali lililo muhimu zaidi ni kulinda roho zao kwa kujiweka mbali na maeneo ya mapigano.
Mapigano baina ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na vile vinavyoitwa Baraza la Mujahid wa Derna yalianza katikati ya mwezi Mei na hadi hivi sasa yameshapelekea raia wasiopungua 17 kuuawa wakiwemo watoto wadogo wawili.
Kwa muda mrefu sasa yaani tangu mwezi Februari 2011, mji wa Derna wa mashariki mwa Libya unadhibitiwa na kundi lalinalojiita kwa jina la Baraza la Mujahid wa Derna, ambalo ni moja ya matawi ya mtandao ya kigaidi wa al Qaida huko nchini Libya.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kuung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Marekani na nchi za Magharibi ziliivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, zikafanya uharibifu wa kupindukia kwenye miundombinu ya nchi hiyo na baadaye kuitelekeza nchi huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi hasimu. Tangu wakati huo hadi leo hii Libya haijawahi kushuhudia utilivu hata siku moja kutokana na kila kundi kuendelea kupigania nafasi kubwa zaidi nchini humo.