Jun 13, 2018 02:41 UTC
  • Vinara wawili wa waasi Ethiopia warudi nyumbani baada ya mazungumzo na serikali

Viongozi wawili wa kundi la waasi wa Ethiopia wamerudi nyumbani baada ya kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed Ali..

Shirika la habari la Ethiopia ENA limeripoti kuwa Yonatan Dubissa na Abebe Geresu waliokuwa wanafanya operesheni zao kutokea nchi jirani ya Eritrea, baada ya kujiunga na kundi haramu la Oromo Liberation Front OLF, wamerudi nyumbani baada ya kufanya mazungumzo na waziri mkuu.

Ripoti zinasema wawili hao ambao walikuwa upande wa serikali kabla ya kujiunga na kundi la waasi, walianza mazungumzo na waziri mkuu mpya wa Ethiopia baada ya kushuhudia mabadiliko ya kisiasa nchini humo.

Mwezi uliopita pia, Serikali ya Ethiopia ilitoa msamaha kwa Andargachew Tsige  kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo ambaye pia ana uraia wa Uingereza ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo. Hiyo ilikuwa ni hatua mpya ya mlolongo wa utoaji msamaha na kuwaachia huru wapinzani iliyochukuliwa na serikali hiyo baada ya miaka kadhaa ya machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo.

Maelfu ya wafungwa, wakiwemo viongozi kadhaa waandamizi wa upinzani wameachiwa huru nchini Ethiopia tangu mwezi Januari mwaka huu. Watu hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya ugaidi au kuchochea kuipindua serikali.

Misamaha hiyo ni sehemu ya mageuzi yaliyoahidiwa kutekelezwa na serikali ya Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo Ahmed Ali.

Hayo yanajiri pia wakati ambao serikali ya Ethiopia imeafiki kutekeleza makubaliano ya suluhu yaliyofikiwa baina yake na Eritrea kwa lengo la kuhitimisha vita na mapigano ya mpakani kati ya nchi mbili.

Tags