Jun 19, 2018 03:53 UTC
  • UN yalaani mashambulizi ya Boko Haram yaliyowalenga Waislamu nchini Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram yaliyowalenga Waislamu waliokuwa wakisherehekea sikukuu ya Idul Fitr kaskazini mashariki mwa Nigeria

Stéphane Dujarric, msemaji wa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  amesema kuwa, mashambulizi yaliyofanywa na magaidi wa Boko Haram dhidi ya raia wa Nigeria ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu na inabidi wahusika wakamatwe na kupandishwa kizimbani.

Magaidi wa Boko Haram na kiongozi wao Abubakar Shekau

 

Siku chache zilizopita, Waislamu wasiopungua 31 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika miripuko miwili ya mabomu iliyotokea wakati Waislamu walipokuwa katikati ya sherehe za sikuuu ya Idul Fitr katika mji wa Damboa, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa, katika mashambulizi hayo wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliilenga mikusanyiko wa Waislamu ambao walikuwa wanarejea majumbani mwao baada ya pirikapirika za sherehe za Idul Fitr yapata saa tano kasorobo usiku, katika vitongoji vya Shuwari na Abachari mjini Damboa katika jimbo Borno ambalo wakati fulani lilikuwa ngome ya magaidi wa Boko Haram.

Boko Haram wamefanya uharibifu mkubwa katika nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon

 

Habari zaidi zilisema kuwa, baada ya magaidi waliokuwa wamejifunga mabomu kujiripua kwenye mikusanyiko hiyo ya Waislamu hao, magaidi wenzao ambao walikuwa mbali kidogo na eneo la tukio walianza kuvurumisha maguruneti katikati ya makundi ya Waislamu ili kuongeza idadi ya wahanga.

Babakura Kolo, mmoja wa makamanda wa genge hilo la ukufurishaji akizungumza kutoka Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, alikiri kuhusika na jinai hiyo na kujigamba kwa kusema: "Hakuna anayehitaji kuambiwa kwamba hiyo ni kazi ya Boko Haram."

Tokea kundi la kigaidi la Boko Haram lianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu zaidi ya 20 elfu wameuawa, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa kundi hilo.

 

Tags