Mapigano yaripotiwa kuendelea kwenye Hilali ya Mafuta, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46156-mapigano_yaripotiwa_kuendelea_kwenye_hilali_ya_mafuta_libya
Msemaji wa Jeshi la Libya amesema kuwa mapigano bado yanaendelea kati ya jeshi hilo la makundi ya waasi katika eneo linalojulikana kama Hilali ya Mafuta nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 21, 2018 23:15 UTC
  • Mapigano yaripotiwa kuendelea kwenye Hilali ya Mafuta, Libya

Msemaji wa Jeshi la Libya amesema kuwa mapigano bado yanaendelea kati ya jeshi hilo la makundi ya waasi katika eneo linalojulikana kama Hilali ya Mafuta nchini humo.

Ahmad al Mismari amesema kuwa, mapigano yangali yanaendelea katika eneo hilo na kwamba jeshi la Libya linaendelea kulipekua eneo la Hilali ya Mafuta kwa shabaha ya kutegua mabomu na mada za miripuko. 

Mapigano katika eneo hilo yalianza Alkhamisi ya tarehe 14 Juni baada ya kamanda wa zamani wa kikosi cha gadi ya kulinda taasisi za mafuta nchini Libya, Ibrahim al Khadhran kusema kuwa yuko tayari kushambulia eneo hilo lenye utajiri wa mafuta kwa kile alichosema ni kukomesha dhulma dhidi ya wakazi wa maeneo hayo. 

Jumamosi tarehe 16 Juni Shirika la Taifa la Mafuta nchini Libya liliwataka wapiganaji wa al Khadhran kuondoka bila ya masharti yoyote katika bandari za mafuta za nchi hiyo. 

Libya

Eneo la Hilali ya Mafuta nchini Libya linajumuisha Bandari za Ras Lanuf, al Sider, Brega na Zueitina.

Mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo yamepunguza uzalishaji na uuzaji nje wa mafuta ya Libya na kwenda chini ya zaidi ya nusu ya kiwango cha kawaida.