Jun 23, 2018 04:09 UTC
  • Genge la waasi nchini Ethiopia lasimamisha operesheni zake

Kundi la waasi la Patriotic Ginbot7 (PG7) la Ethiopia limetangaza uamuzi wa upande mmoja wa kusimamisha kwa muda usiojulikana operesheni zake zote za utumiaji silaha katika maeneo yote ya nchi.

Katika taarifa, kundi hilo la wapiganaji limetangaza kuwa: Uamuzi huu wa kusimamisha harakati za kujilinda kwa kutumia silaha kuanzia Juni 22 ni hatua chanya tuliyochukuwa ili kuonyesha utayarifu wetu wa kuzima jitihada zozote za kukwamisha msururu wa mageuzi unaofanywa hivi sasa na chama tawala EPRDF. 

Haya yanajiri siku chache baada ya viongozi wawili wa kundi la waasi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, Yonatan Dubissa na Abebe Geresu waliokuwa wanafanya operesheni zao kutokea nchi jirani ya Eritrea, baada ya kujiunga na kundi haramu la Oromo Liberation Front OLF, kurudi nyumbani baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed.

Mwezi uliopita pia, serikali ya Ethiopia pia ilitoa msamaha kwa Andargachew Tsige,  kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo ambaye pia ana uraia wa Uingereza ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo. Hiyo ilikuwa ni hatua mpya ya mlolongo wa utoaji msamaha na kuwaachia huru wapinzani iliyochukuliwa na serikali hiyo baada ya miaka kadhaa ya machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo.

Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia, Ahmed Ali.

Maelfu ya wafungwa, wakiwemo viongozi kadhaa waandamizi wa upinzani wameachiwa huru nchini Ethiopia tangu mwezi Januari mwaka huu. Watu hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya ugaidi au kuchochea kuipindua serikali.

Misamaha hiyo ni sehemu ya mageuzi yaliyoahidiwa kutekelezwa na serikali ya Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo Ahmed Ali.

Tags