Karibu wahajiri elfu moja wazuiwa kusafiri katika fukwe za Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46308-karibu_wahajiri_elfu_moja_wazuiwa_kusafiri_katika_fukwe_za_libya
Karibu wahajiri elfu moja waliokuwa mbioni kupanda mitumbwi kuelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean wamezuia kusafiri katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kwenye fukwe za Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2018 10:07 UTC
  • Karibu wahajiri elfu moja wazuiwa kusafiri katika fukwe za Libya

Karibu wahajiri elfu moja waliokuwa mbioni kupanda mitumbwi kuelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean wamezuia kusafiri katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kwenye fukwe za Libya.

Gadi ya ulinzi wa fukweni ya Libya imetangaza kuwa, wahajiri 490 haramu wamekamatwa katika fukwe za al Qura Bolelli na kupelekewa mjini Tripoli kwa kutumia meli ya jeshi la majini la Libya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la majini la Libya, kundi jingine la wahajiri haramu lililokuwa na watu 361 wakiwemo wanawake 88 na watoto wadogo 44 limekamatwa katika fukwe za al Khoms. Kabla ya hapo pia wahajiri wengine 97 walikuwa wamekamatwa kwenye eneo hilo hilo.

Wahajiri haramu wanaishi katika mazingira magumu sana nchini Libya

 

 

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 21 Juni pia, jeshi la majini la Libya lilitangaza habari ya kuongezeka kupindukia idadi ya mitumbwi inayobeba wahajiri haramu na hatari kubwa zinazoikabili mitumbwi hiyo ya plastiki ambayo aghlabu yake huwa inapinduka na waliomo ndani yake kufa maji.

Libya ndiyo njia kuu inayotumiwa na wahajiri haramu hasa Waafrika wenye tamaa ya kufika barani Ulaya.

Kukosekana serikali kuu yenye nguvu na ukosefu mkubwa wa usalama nchini Libya umetoa mwanya kwa magenge ya magendo ya binadamu kutumia vibaya fursa hiyo kuingiza kila mwaka makumi ya maelfu ya wahajiri haramu nchini Libya. Sehemu kubwa ya wahajiri hao haramu huwa hawafiki wanakokwenda na huishia kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni kama bidhaa au kutumbukia mikononi mwa magenge ya kigaidi.