Polisi ya Tanzania yawatia mbaroni wezi wakubwa wa mitandao ya simu
Jeshi la polisi maalamu ya Dar es salaam nchini Tanzania limetanza kuwa, linawashikilia watu 15 kwa kujihusisha na wizi kwa njia ya mtandao.
Akizungumza Jumatano ya leo kaimu kamanda wa polisi kanda maalum, Naibu Kamishna wa jeshi la polisi, Liberatusi Sabasi, amesema kuwa watuhumiwa hao wametiwa mbaroni baada ya kufanyika msako kwa kipindi cha siku saba katika maeneo tofauti ya ndani na nje ya mji huo. Sabasi amefafanua kuwa, jeshi hilo lilifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa watu mbalimbali ambao wamekuwa wakipokea ujumbe mfupi wa maneno ukiwashawishi kutuma pesa kwenye namba nyingine.
Amezidi kufafanua kuwa, miongoni mwa wezi hao, ni pamoja na Lule Lusale (35) mkazi wa Rgani Ng’ambo ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa kundi hilo na kwamba amekutwa na simu 45, kadi za simu 352, vitambulisho kadhaa na komputer mpakato tano (laptops). Katika kipindi cha kuanzia Aprili mwaka huu kumekuwa na jumbe fupi za maneno ambazo zimekuwa zikitumwa kwa watu mbalimbali zenye maneno yanayosema: “Nitumie hiyo hela katika namba hii”, “Namba ile ya awali ina matatizo nitumie sasa hivi” na meseji nyingine ikisema Mganga wa jadi msamaria, je unasumbuliwa na magonjwa sugu, ndoa, pesa na majini wasiliana kwa namba 0742138389 huduma itakufuata ulipo. Kwa mujibu kamanda Liberatusi Sabasi, wahalifu hao walikuwa wakitumia mfumo wa Bulk SMS ambao unawawezesha kutuma jumbe zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja na kuwaendea watu wengi na kuwaibia fedha zao, suala ambalo lilililazimu jeshi hilo kuanzisha operesheni hiyo.