Jeshi la Libya latangaza kukomboa kikamilifu mji wa Derna
Vikosi vya Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar vimetangaza kuwa vimeshafanikiwa kukomboa kikamilifu mji wa Derna ulioko mashariki mwa nchi hiyo.
Akitoa tangazo hilo jana Alkhamisi kwa njia ya televisheni, Jenerali Haftar amesema: Tunaona fahari kutangaza kukombolewa mji wa Derna.
Amewaahidi wakazi wa mji huo juu ya kufunguliwa ukurasa mpya wa amani, usalama na uhuru baada ya kukombolewa mji huo wa kistratajia ambao umeshuhudia makabiliano makali ya kuukomboa tokea Mei 7.
Mapema mwezi huu, Ahmad al Mismari, Msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya alisema kuwa jeshi hilo linadhibiti asilimia 80 ya mji wa Derna, na vimefikia kiwango cha kutiwa nguvuni na kukamatwa makamanda wa makundi ya kigaidi.
Mapigano baina ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na vile vinavyoitwa Baraza la Mujahid wa Derna yalianza katikati ya mwezi Mei na hadi hivi sasa yameshapelekea raia wasiopungua 17 kuuawa wakiwemo watoto wadogo wawili.
Libya imekuwa katika machafuko makubwa ya ndani na mapigano ya makundi ya kigaidi tangu mwaka 2011 wakati vikosi vya jeshi la NATO vikisaidiwa na Marekani vilipoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kupelekea kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.