Jenerali Khalifa Haftari aonya kuhusu kuweko majeshi ya kigeni Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46460-jenerali_khalifa_haftari_aonya_kuhusu_kuweko_majeshi_ya_kigeni_libya
Jenerali Khalifa Haftari, kamanda wa kikosi kinachojulikana kama Jeshi la Taifa la Libya ameonya kuhusiana na kuweko kwa vikosi vya kigeni kusini mwa nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na uhajiri haramu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2018 03:11 UTC
  • Jenerali Khalifa Haftari aonya kuhusu kuweko majeshi ya kigeni Libya

Jenerali Khalifa Haftari, kamanda wa kikosi kinachojulikana kama Jeshi la Taifa la Libya ameonya kuhusiana na kuweko kwa vikosi vya kigeni kusini mwa nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na uhajiri haramu.

Jenerali Khalifa Haftari amesema hayo katika radiamali yake kwa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na kuainishwa maeneo ya kuwapeleka nje ya Ulaya wahajiri wa Kiafrika walioingia barani humo.

Kamanda huyo wa Jeshi la Taifa la Libya amesisitiza kuwa, nchi yake haitakubaliana na uwepo wa wanajeshi wa kigeni katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, juzi vikosi vya Jeshi la Taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar vilitangaza kuwa vimeshafanikiwa kukomboa kikamilifu mji wa Derna ulioko mashariki mwa nchi hiyo.

Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa Libya

Mapigano baina ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na vile vinavyoitwa Baraza la Mujahid wa Derna yalianza katikati ya mwezi Mei na hadi hivi sasa yameshapelekea raia wasiopungua 17 kuuawa wakiwemo watoto wadogo wawili.

Libya imekuwa katika machafuko makubwa ya ndani na mapigano ya makundi ya kigaidi tangu mwaka 2011 wakati vikosi vya jeshi la NATO vikisaidiwa na Marekani vilipoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kupelekea kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.

Kwa sasa nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa amani na changamoto ya wahajiri wa Kiafrika wanaopitia nchini humo wakielekea barani Ulaya.