Wafanyakazi wauawa katika kituo cha maji nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46622-wafanyakazi_wauawa_katika_kituo_cha_maji_nchini_libya
Wabeba silaha wasiojulikana wamewapiga risasi na kuwaua wafanyakazi wawili na kuwateka nyara wengine wawili katika kituo cha kusambaza maji kusini mashariki mwa Libya mapema leo asubuhi. Shambulizi hilo ni la pili kulenga vituo vya kusambaza maji nchini humo katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2018 13:40 UTC
  • Wafanyakazi wauawa katika kituo cha maji nchini Libya

Wabeba silaha wasiojulikana wamewapiga risasi na kuwaua wafanyakazi wawili na kuwateka nyara wengine wawili katika kituo cha kusambaza maji kusini mashariki mwa Libya mapema leo asubuhi. Shambulizi hilo ni la pili kulenga vituo vya kusambaza maji nchini humo katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Katika taarifa, Shirika la Mradi wa Mto Mkubwa wa Kujitengenezea  limesema kuwa magaidi wametekeleza hujuma katika eneo la Tazirbu ambapo wameibua ghasia na kisha wakapora mali na kuua raia huku wakieneza wahka na hofu miongoni mwa familia na watoto wa wafanyakazi ambao huhakikisha maji yanafika katika miji. Mradi huo wa maji ni muhimu katika kusambaza maji katika Jangwa la Sahara nchini Libya.

Taarifa zinasema mhandisi na mlinzi ni miongoni mwa waliouawa katika tukio hilo huku walinzi wawili wakitekwa nyara. Washambuliaji hao pia waliiba magari na vyakula katika eneo hilo.

Magaidi wa ISIS

Siku ya Ijumaa watu wasiojulikana waliwateka nyara raia watatu wa Ufilipino na Mkorea ambao walikuwa wakifanya kazi kama wahandisi katika kituo cha Al Hassouna ambacho ni sehemu ya mtandao wa kusambaza maji katika jangwa la Libya.

Haijabainika ni nani aliyetekeleza mashambulizi hayo mawili lakini inaaminika kuwa magaidi wakufurishaji wanaofungamana na al-Qaeda au ISIS  walio katika jangwa la Libya yamkini ndio waliotekeleza hujuma hizo.