Mripuko wa bomu watokea karibu na ikulu ya rais wa Somalia
Polisi ya Somalia imetangaza habari ya kutokea mripuko wa bomu karibu na ikulu ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa nchi hiyo mjini Mogadishu.
Taarifa iliyotolewa na polisi ya mjini Mogadishu imesema kuwa, gaidi mmoja amejiripua ndani ya gari karibu na ikulu ya rais na kwamba hadi sasa bado idadi kamili ya hasara iliyotokana na hujuma hiyo haijatangazwa, ingawa baadhi ya duru za habari zinasema kuwa kwa akali watu tisa wamepoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi wa Mogadishu, maafisa usalama wa Somalia walichukua hatua ya kufyatua risasi ambapo muda punde baadaye kulijiri mripuko mwingine wa bomu karibu na kituo cha upekuzi cha polisi.

Tayari kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab lenye mafungamano na genge la al-Qaidah, limetangaza kuhusika na miripuko hiyo. Kundi hilo limekuwa likidhibiti baadhi ya maeneo hususan ya vijijini nchini Somalia, kuanzia mwaka 2011. Hatua za jeshi la Somalia kwa ajili ya kudhibiti maeneo hayo bado hazijazaa matunda na badala yake, hujuma za kigaidi za genge hilo zimeshadidisha machafuko nchini humo na nchi nyingine jirani. Somalia imekuwa uwanja wa vitendo vya ukatili na mauaji tangu muongo wa 90 yaani tangu kupinduliwa serikali ya Mohamed Siad Barre, rais wa zamani wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.