Baraza la Usalama kupasisha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46722-baraza_la_usalama_kupasisha_vikwazo_vya_silaha_dhidi_ya_sudan_kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa wiki hii kupasisha pendekezo la kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan Kusini, siku chache baada ya pande hasimu katika mgogoro wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kukubaliana kusitisha vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 12, 2018 00:11 UTC
  • Baraza la Usalama kupasisha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa wiki hii kupasisha pendekezo la kuiwekea vikwazo vya silaha Sudan Kusini, siku chache baada ya pande hasimu katika mgogoro wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kukubaliana kusitisha vita.

Rasimu ya azimio hilo inataka vikwazo hivyo vya silaha vianze kutekelezwa kuanzia mwezi huu hadi Mei 31 mwaka ujao 2019.

Vikwazo vipya vya silaha dhidi ya Sudan Kusini vimetangazwa licha ya mrengo wa upinzani nchini humo na serikali kufikia makubaliano ya amani nchini Uganda, baada ya kikao cha nchi jirani ya Sudan kugonga mwamba.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za binadamu, pande mbili hizo hasimu nchini Sudan Kusini zimehusika katika mauaji ya ulipizaji kisasi ambayo yaliibua migawanyiko ya kikabila.

Wapiganaji watiifu kwa Rais Salva Kiir

Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kufuatia machafuko hayo.

Vita hivyo vilianza mwaka 2013 baada ya hitilafu za kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kusababisha machafuko ya ndani.