China: Nchi za Afrika zijiepushe kuwaingiza madarakani wala rushwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46845-china_nchi_za_afrika_zijiepushe_kuwaingiza_madarakani_wala_rushwa
Mkuu wa Idara ya Kimataifa na Waziri wa Mahusiano wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti nchini China (CPC), Song Tao, amezishauri serikali za mataifa ya bara la Afrika kuandaa mkakati maalumu ambao kwa mujibu wake utazuia viongozi wala rushwa kuingia madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2018 14:12 UTC

Mkuu wa Idara ya Kimataifa na Waziri wa Mahusiano wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti nchini China (CPC), Song Tao, amezishauri serikali za mataifa ya bara la Afrika kuandaa mkakati maalumu ambao kwa mujibu wake utazuia viongozi wala rushwa kuingia madarakani.

Tao amesema kuwa ni suala lisilowezekana kwa nchi hizo kufikia uchumi wa kati iwapo viongozi wanaopenda kula rushwa wataachwa wagombee na hatimaye kuingia madarakani. Kiongozi wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti nchini China ameyasema hayo katika mkutano wa kimataifa wa vyama vya siasa uliovikutanisha zaidi ya vyama 40 kutoka nchi tofauti za Afrika jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine ameashiria namna ambavyo China iliamua kuanzisha kamati za ukaguzi na usimamizi ambazo zilisaidia kuwabana viongozi wazembe na wala rushwa.

Rais John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Guo Songiang

Amesisitiza kwamba hakuna njia itakayozisaidia nchi za Afrika kupata maendeleo kiuchumi kama suala la kudhibiti rushwa halitawekewa mikakati madhubuti. "Inawezekana Afrika ikadhibiti rushwa. Msiruhusu viongozi wala rushwa, hawa ni hatari sana kwa maendeleo", amesema Song Tao. Kwa mujibu wa Kiongozi wa Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti nchini China (CPC), kuna udharura wa kila nchi kuwa na chombo cha kudhibiti rushwa chenye uwezo wa kuzuia, kuwakamata, kuwachunguza, kuendesha mashtaka na kisha kuwafilisi mali zao zote zilizopatikana kwa rushwa.

Mkutano wa kimataifa unaoviunganisha zaidi ya vyama 40 vya siasa vya Afrika na CPC unalenga kuandaa misingi imara ya kiuchumi na ushirikiano kati ya vyama hivyo.