Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania: Wafungwa wataanza kujilisha wenyewe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46923-waziri_wa_mambo_ya_ndani_tanzania_wafungwa_wataanza_kujilisha_wenyewe
Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Tanzania, Kangi Lugola, amemtaka Mkuu wa Magereza nchini humo, Kamishna Jenerali Phaustine Martin Kasike kumpelekea mikakati ya kuhakikisha wafungwa wanajilisha kwa kufanya kazi badala ya kulishwa kwa fedha za serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2018 10:07 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania: Wafungwa wataanza kujilisha wenyewe

Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Tanzania, Kangi Lugola, amemtaka Mkuu wa Magereza nchini humo, Kamishna Jenerali Phaustine Martin Kasike kumpelekea mikakati ya kuhakikisha wafungwa wanajilisha kwa kufanya kazi badala ya kulishwa kwa fedha za serikali.

Lugola ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, Rais John Magufuli wa nchi hiyo amechoka kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuwalisha wafungwa na wahalifu badala ya kuhudumia wananchi kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu, reli, ndege, na miradi ya umeme. “Rais ameniagiza kuhakikisha magereza yote nchini, wafungwa wanajilisha kwa kutumia nguvu zao na kuwa sehemu ya kujutia kile walichokifanya kwenye jamii, siyo wanafungwa halafu wanakaa tu, wanalishwa, wanarudi wakiwa na vitambi, amesema waziri huyo na kusisitzia kuwa amemwelekza Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini humo kutengeneza mkakati maalumu wa kuhakikisha wafungwa wote nchini wanajilisha kuanzia mboga, kama ni kufuga samaki au kulima maharage, na kusiwe na kisingizio chochote kwani jambo hili linatekelezeka.

Wafungwa watatakiwa kufanya kazi zaidi ili kujilisha

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania amesema Bunge lijalo tutaanza na kubadilisha sheria ili kusiwe na kinga kwa wafungwa, wafanye kazi, wajilishe na wawalishe mahabusu, na ikiwezekana magereza iweze kupata chakula cha ziada kinachoweza kuuza na kutengeneza kipato.  Katika sehemu nyingine Lugola ameonyesha kukerwa na tabia ya wafungwa kuingiza vitu magerezani na kusema: “Rais Magufuli amekerwa na vitedo vya wafungwa kuingia na vitu magerezani mfano simu za mkononi na kwamba amemwagiza Mkuu wa Magereza kudhibiti suala hilo. 

Hivi karibuni shirikisha la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilimkosoa vikali Rais John Magufuli wa Tanzania kwa kutaka wafungwa nchini humo kufanyishwa kazi usiku na mchana na kupigwa mijeledi wakiwa wavivu. Amina Hersi, afisa wa Amnesty katika kanda ya Afrika Mashariki alisema kuwa, matamshi hayo ya Rais John Magufuli ni ya kikatili na yasiyo na chembe ya utu.