Madereva 11 wa taxi Afrika Kusini wapigwa risasi na kuuawa wakitoka mazishini
Maderva 11 wa taxi wamepigwa risasi na kuuawa nchini Afrika Kusini wakati wakirejea mjini Johannesburg baada ya kuhudhuria mazishi ya mwenzao katika eneo la Kwa-Zulu Natal.
Madereva hao walikuwa wanachama wa Jumuiya ya Taxi ya Guateng na walikuwa ndani ya basi katika barabara ya R74 wakati watu wasiojulikana walipowavizia na kuwafyatulia risasi.
Msemaji wa Polisi katika eneo la Kwa-Zulu Natal Jay Naicker amesema ufyatuaji risasi huo ulijiri saa mbili usiku jana kwa saa za Afrika Kusini na kwamba mbali na madereva 11 kuuawa wengine wane walijeruhiwa vibaya na wamelazwa hospitalini.
Amesema kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na mzozo na mapigano baina ya madereva wa taxi katika eneo hilo na kwmaba uchunguzi ungali unaendelea.

Taxi ambazo ni sawa na matatu nchini Kenya au daladala nchini Tanzania hutumiwa na wananchi waliowengi Afrika Kusini katika usafiri na kwa kawaida machafuko huibuka baina ya makundi hasimu yanayotaka kudhibiti usafiri katika njia zenye faida kubwa.